Leading Centre of Excellence for Knowledge, Skills, and Applied Education in Science and Technology
Ndaki ya Usanifu Majengo na Teknolojia ya Majenzi (College of Architecture and Construction Technology - CoACT) imezindua Klabu ya Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Change Action Club) ikiwa ni sehemu ya utunzaji wa mazingira na kupunguza changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Uzinduzi wa Klabu hiyo ulifanyika tarehe 23 Aprili 2024 na Rasi wa Ndaki hiyo Dkt. Mwajuma Lingwanda huku ukihudhuriwa na wanataaluma na wanafunzi kutoka katika Ndaki hiyo.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa Klabu hiyo, Rasi wa Ndaki ya Usanifu Majengo na Teknolojia ya Majenzi Dkt. Mwajuma Lingwanda alisisitiza juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kuwa na hewa nzuri, kupata kivuli na kupunguza hewa ukaa.
Hivyo aliwaomba wanafunzi, pamoja na wanataaluma kujenga utamaduni wa kupanda miti nyumbani, maeneo ya ofisini na katika kila eneo ambalo linatakiwa kupanda miti, huku akibainisha kuwa suala la upandaji miti ni jambo lenye kheri kwa kila mwanadamu atakaefanya hivyo.
Uzinduzi wa Klabu hiyo ulienda sambamba na zoezi la upandaji miti katika baadhi ya maeneo ya Chuo ikiwemo eneo la Hosteli 8D na 8C na katika maeneo ya kusomea (vimbwete) ambapo zaidi ya miti 100 ilipandwa katika maeneo yaliyotajwa.
Ndaki ya Usanifu Majengo na Teknolojia ya Majenzi (CoACT) ni miongoni mwa Ndaki sita zilizo ndani ya Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ikiwa ni Ndaki ya kwanza kuanzisha na kusimamia Klabu inayojihusisha moja kwa moja na mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.