Leading Centre of Excellence for Knowledge, Skills, and Applied Education in Science and Technology
Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimeshuhudia tukio la kihistoria baada ya viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi (MUSTSO) kuapishwa rasmi kuanza majukumu yao kwa mwaka wa masomo 2026/2027. Katika hafla hiyo iliyofanyika chuoni hapo, Bw. George Gabriel Ndendya alitwaa kiapo cha uongozi kama Rais wa MUSTSO, huku Bi. Grace Sawile Kavile akiwa Makamu wake. Mbali na viongozi hao wawili, Mwenyekiti wa Mahakama ya Serikali ya Wanafunzi, Makamu Mwenyekiti na Katibu wa Mahakama pia waliapishwa rasmi, kukamilisha muundo wa uongozi wa serikali hiyo kwa mwaka ujao.
Akihutubia kama mgeni rasmi wa hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Aloys Mvuma, aliwapongeza viongozi wapya kwa kuaminiwa na wenzao na kuwataka kutambua mipaka ya mamlaka yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za chuo. Alizitaja nguzo nne ambazo serikali mpya inapaswa kuzijenga juu yake, nazo ni utawala bora, uwazi, uwajibikaji na haki katika kuwahudumia wanafunzi wote. "Pamoja na majukumu ya uongozi, masomo yenu lazima yabaki kipaumbele. Lengo kuu la uwepo wenu chuoni ni kupata elimu na ujuzi," alisema Prof. Mvuma, huku akiwaomba wazazi na walezi waliohudhuria kuendelea kuwahamasisha watoto wao kujikita katika taaluma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Bi. Nuru Muharami Manyara, alieleza kwamba mchakato wote wa uchaguzi uliendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na ushirikishwaji wa wanafunzi. Alipongeza wajumbe wa tume kwa weledi na uzalendo wao katika kutekeleza wajibu huo muhimu. Mkuu wa Idara ya Huduma za Wanafunzi, Bw. Keneth Mwampashe, alithibitisha kwamba ijapokuwa ushindani ulikuwa mkubwa, uchaguzi ulifanyika kwa amani na uwazi. Alitoa wito kwa viongozi wapya kuachana na tofauti za kisiasa zilizojitokeza wakati wa kampeni na kuumba serikali ya umoja itakayowahudumia wanafunzi wote bila ubaguzi.

Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Bw. Agustino Matem, aliwataka viongozi hao kuongoza kwa uadilifu na kuepuka upendeleo katika uteuzi wa watendaji watakaowasaidia kuendesha serikali, akisisitiza kuwa ukweli, uwazi na uwajibikaji ni nguzo kuu za uongozi bora. Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Fedha, Uongozi na Mipango, Dkt. Juma Said Ally, aliwashauri viongozi hao kuhakikisha mipango yao inakwenda sambamba na mipango ya chuo ili kuepusha migongano ya ratiba na kuwezesha ushirikiano mzuri. Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Dkt. Yazid Hassan Mwishwa, aliwataka viongozi hao kuwa mabalozi wa taaluma kwa kuwahamasisha wanafunzi wenzao kuhudhuria vipindi na kujifunza kwa bidii.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya viongozi wote walioapishwa, Rais wa MUSTSO, Bw. George Gabriel Ndendya, aliahidi kushirikiana kwa ukamilifu na Menejimenti ya Chuo katika kutekeleza majukumu yake. Alisema serikali yake itafanya kazi kwa bidii na kujituma kuwatumikia wanafunzi wote na kuchangia kuifanya MUST kuwa mazingira bora zaidi ya kujifunzia. "Nawashukuru wanafunzi wenzangu kwa imani waliyonipa. Nitaitumia fursa hii kwa moyo wote kuwatumikia," alisema Ndendya.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa matumaini makubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, wote wakionyesha imani yao kwa uongozi mpya katika kuendeleza ustawi na maendeleo ya wanafunzi wa MUST kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

