Leading Centre of Excellence for Knowledge, Skills, and Applied Education in Science and Technology
Taasisi ya Kuzui ana Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imeendesha mafunzo ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa watumishi wa MUST Kampasi ya Mbeya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwajibikaji, uadilifu na utoaji bora wa huduma kwa wadau mbalimbali wa chuo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika chuoni hapo yalifunguliwa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Aloys Mvuma, ambaye alisisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa uwazi na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Prof. Mvuma alisema kuwa MUST ina jukumu kubwa la kuandaa na kusimamia rasilimali watu wenye weledi, maadili na uzalendo katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya taifa. Alieleza kuwa pamoja na jukumu la msingi la kutoa elimu ya juu, chuo pia hutoa huduma mbalimbali kwa watumishi, wanafunzi na jamii inayokizunguka ikiwemo huduma za ushauri, afya, malazi na huduma nyingine muhimu.
“Ubora wa huduma hizi unategemea uwepo wa mifumo imara ya uwajibikaji na maadili. Hivyo, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa rushwa haina nafasi katika taasisi yetu kwa kuwa inaweza kuathiri utoaji wa huduma na kuharibu taswira ya chuo,” alisema Prof. Nmvuma.
Aidha, aliwataka watumishi wa chuo kuwa mabalozi wa maadili mema kwa kutoruhusu vitendo vya rushwa kujengeka katika maeneo yao ya kazi. Alibainisha kuwa chuo kinaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), katika kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na utawala bora.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Emmanuel Jilungu kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, alieleza kuwa rushwa ni moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha haki, maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa kila mtumishi wa umma ana wajibu wa kisheria na kimaadili wa kukemea, kupinga na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa pindi vinapotokea. Aliongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.
“Rushwa ni adui wa haki na maendeleo. Inapunguza ufanisi wa taasisi na kudhoofisha imani ya wananchi kwa watoa huduma. Hivyo kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anakuwa sehemu ya suluhisho kwa kuzingatia maadili na sheria,” alisema Wakili Jilungu.
Akitoa salamu za kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya uongozi wa chuo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Dkt. Juma Ally, aliwashukuru wawezeshaji na washiriki kwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.

Dkt. Ally aliwataka watumishi waliohudhuria kutumia maarifa na uelewa walioupata katika kuboresha utendaji wao wa kazi na kuendelea kuwa mabalozi wa maadili mema katika maeneo yao ya kazi. Vilevile, aliwahimiza kuyasambaza maarifa hayo kwa watumishi wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki kutokana na majukumu mbalimbali.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati endelevu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ya kujenga mazingira ya kazi yanayozingatia uwazi, uwajibikaji, uadilifu na utawala bora, sambamba na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa watumishi, wanafunzi na jamii zinakuwa na ubora unaostahili.