What do you want to learn?

Browse all programmes  
No programmes matching {{ filters.name }}

News

Home | News | Naibu Katibu Wizara Atembelea MUST: Teknolojia Ndiyo Jibu la Kilimo cha Kesho

Naibu Katibu Wizara Atembelea MUST: Teknolojia Ndiyo Jibu la Kilimo cha Kesho

Naibu Katibu Wizara Atembelea MUST: Teknolojia Ndiyo Jibu la Kilimo cha Kesho

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia masuala ya kilimo, Profesa Peter Msoffe, amefanya ziara ya kikazi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), huku akisisitiza umuhimu mkubwa wa teknolojia katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania. Ziara hiyo inachukuliwa kama hatua muhimu katika juhudi za serikali za kuunganisha elimu ya juu na mahitaji halisi ya sekta ya kilimo, sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.

Akizungumza baada ya kuwasili chuoni hapo, Profesa Msoffe alisema ziara hiyo inalenga kutathmini mchango wa chuo katika kuzalisha wataalamu wanaohitajika na sekta ya kilimo, pamoja na kuchunguza fursa za ushirikiano katika teknolojia na uvumbuzi. "Kilimo cha kisasa kinategemea sana teknolojia na vifaa. Ujio wangu hapa ni kuona namna wizara yetu inavyofaidika na wataalamu wanaozalishwa hapa, lakini pia kuona namna teknolojia na bunifu mbalimbali zinavyoweza kusaidia sekta nzima ya kilimo. Nimefurahi sana kuwa mahali hapa," alisema Profesa Msoffe.

Katika ziara hiyo, Katibu alipita katika maeneo mbalimbali ndani ya chuo, ikiwemo karakana, maabara na viwanda, akizungumza moja kwa moja na watafiti, wahadhiri na wanafunzi ili kuelewa vyema jinsi chuo hiki kinavyojibu changamoto za sekta mabalimbali ikiwemo sekta ya kilimo. Katika karakana, alishuhudia utengenezaji wa zana mbalimbali, huku maabara zikimpa fursa ya kuona utafiti unaoendelea katika Nyanja mbalimbali za sayansi. Kwa upade wa kiwanda alijionea uhalisia wa uzalishaji na ubunifu wa teknolojia unaofanyika ndani ya taasisi hii.

MUST ni miongoni mwa vyuo vikuu vinavyojikita katika taaluma za teknolojia na uhandisi nchini Tanzania. Chuo hiki si tu kitovu cha elimu, bali pia ni nyumba ya zana na teknolojia maalum zinazohusiana moja kwa moja na sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo, kuanzia mashine hadi mifumo ya umwagiliaji na usindikaji. Ushirikiano kati ya wizara na taasisi kama MUST unatarajiwa kuharakisha upatikanaji wa teknolojia bora kwa wakulima na hatimaye kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.

mfupi.jpg 319.06 KB
Prof. Prof. Peter Msoffe (Kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo kwenye picha ya pamoja na Prof. Said Ali Vuai, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, alipotembela chuoni hapa

elisha.jpg 350.37 KB
Prof. Peter Msoffe (Kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo akisikiliza maelezo kutoka kwa msimamizi mtendaji wa Kiwanda cha Maziwa MUST.

CITT.jpg 325.42 KB
Prof. Peter Msoffe (Katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, kwenye picha ya pamoja na Prof. Said Ali Vuai, Naibu Makamu Mkuu wa chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri wa kaitaalamu (Kushoto) pamoja na Mr. Cornel Msemwa Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji

Apply Now